Muungano wa wauguzi wajitathmini mafanikio

Muungano wa wauguzi na wakunga walio kwenye huduma binafsi za afya ya uzazi na mtoto vijijini (Prinmat), umekutana na wadau jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kutathmini mafanikio na changamoto zinazoukabili katika kipindi cha mwaka mmoja.

Katibu Mtendaji wa Prinmat, Keziah Kapesa, alisema jana kuwa tathmini ya mafanikio na changamoto iliyofanywa inahusu huduma zilizotolewa na mradi unaomilikiwa na Muungano kuanzia Oktoba, mwaka jana hadi Septemba, mwaka huu.

Mradi huo ujulikanao kama `Ujana’ unaolenga vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 25 waliomo ndani ya ndoa, unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana Ukimwi (Unaids) kupitia asasi ya kimataifa inayojishughulisha na huduma za afya ya familia (FHI).

Kapesa alisema huduma hizo ambazo hutolewa na Prinmat kupitia vituo vyao 11 vilivyomo kwenye mradi huo uliodumu kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2008, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwavutia vijana kupitia michezo mbalimbali ikiwamo mpira na maigizo.

Vituo vilivyomo kwenye mradi vinapatikana katika Wilaya za Kinondoni na Ilala, mkoani Dar es Salaam; Wilaya ya Mkuranga (mkoani Pwani) na Wilaya ya Morogoro Mjini na Kilosa (mkoani Morogoro). Prinmat ina vituo 63 nchini kote.

Hata hivyo, Kapesa alisema katika kipindi hicho wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo namna ya kuwaweka pamoja vijana ili kuwapa elimu kuhusu masuala ya uzazi, mtoto na Ukimwi.

Alisema uamuzi wa mradi huo kulenga vijana waliomo ndani ya ndoa unatokana na uwezekano mkubwa kwa vijana hao kupata Ukimwi na kuambukizana.

Kutokana na hilo, alisema miongoni mwa kazi zinazofanywa na Prinmat ni pamoja na kushawishi mke na mume kuwa huru kujadiliana kuhusu ukimwi, kutumia kinga dhidi ya maradhi hayo na kuwa waaminifu katika ndoa.

SOURCE: NIPASHE

  • Google+
  • PrintFriendly